Jumatatu, 5 Desemba 2016

HISTORIA YA IKIZU NA WAIKIZU SEHEMU YA PILI

                             
                                    II. CHIMBUKO LA WAIKIZU-NYAKINYWA

Historia ya Nyakinywa kama ilivyokuwa kwa Jemedari Muriho Nyikenge inaanzia mbali na vituko vingi ambavyo kwa njia fulani vyafanana  na vya jemedari Muriho. Utangulizi wake, kwa upande mwingine ni tofauti kimsingi na kimtazamo.

Kihistoria inasemekana wazazi wa Nyakinywa walikuwa Wahima na wa ukoo wa kitawala huko sehemu za Uganda, Burundi, Karagwe na Geita. Baba yake Nyakinywa alikuwa mdogo wake mtemi mmoja wapo kati ya maeneo hayo yaliyotajwa. Mzee huyu alikuwa na Ng'ombe wengi sana. Siku moja kwa bahati mbaya ng'ombe wake mmoja alimeza hati za utawala (Ndezi) za kaka yake. Kaka yake alitaka ng'ombe huyo achinjwe ili hati hizo ziweze kuondolowa lakini mdogo wake alilipinga wazo hilo la ng'ombe wake kuchinjwa akiahidi kumtunza na kulisha vizuri ili akinya amrudishie kaka yake. Mtemi hakukubaliana na ombi hilo aliamuru ng'ombe huyo achinjwe na hati hizo ziondolewe na watumishi wake walifanya kadri ya amri ya mtemi alivyoagiza hivyo ng'ombe huyo alichinjwa na hati hizo zilitolewa na kukabidhiwa kwa mtemi. Kitendo hicho kilimuudhi sana mdogo wake ambaye aliamua kuhama, alichukua ng'ombe wake karibu wote akaondoka na watu wake, akasafiri kupitia sehemu nyingi mpaka mwisho na pembeni mwa Usukuma, sehemu iitwayo kwa sasa Kanadi. Huko Kanadi akawa mtawala na nchi ikaneemeka ikawa na ng'ombe wengi na maziwa yakapatikana kwa kuzidi mahitaji. Yakawa yanamwaga ovyo mitoni. Mvua zilipokuwa zinanyesha maziwa hayo yalisafirishwa sehemu za mbali. Mtemi alipoona jambo hilo aliwakataza watu wake wasimwage maziwa mitoni, lakini hawakufuata ushauri wake. Maziwa yaliyokuwa yakimwagwa mitoni yalisafiri hata kufika Umasaini. Wamasai waliyafuatilia mpaka wakafika Kanadi. Ikazuka vita kubwa dhidi ya Wamasai, watu wengi walikufa na Wamasai walichukua ng'ombe wengi na kwenda nao Umasaini.

Hali ya Kanadi ikazidi kuwa ya wasiwasi, hali ya baba yake ikawa mbaya na alipokaribia kuaga dunia alimuita Nyakinywa na dada zake wawili, Wahunda na Wang'ombe awape wosia. Nyumba ya mama Nyakinywa ndiyo ilikuwa na haki kurithi utawala wa nchi, lakini haikuwa na mtoto wa kiume. Hivyo alibashiri fujo kutokea baada ya kufa kwaketoka kwa kaka zake  Nyakinywa wa nyumba nyingine kutaka kuwaua ili wasitawale. Wosia wa baba yao hao wasichana watatu ulisema yeye akifa waondoke Kanadi wasifi mpaka nchi yenye mlima mrefu huko utawala wao unawasubiri. Akawatabiria jinsi watakavyosafiri na mambo yote yatakayowakuta njiani kabla ya kufika mwisho na pia ishara ya mwisho ya mwisho kuwajulisha wamefika safari yao. Mwisho akawaombea na kuwabariki hao wasichana watatu.

Siku chache baadae baba yao alifariki na wakamkalia na kumlilia kama kawaida ya Mtemi anapoaga dunia. Baada ya siku hizo za laziam Nyakinywa na dada zake wawili walichukua hati za utawala, wakatoroka Kanadi na kuanza safari ya mbali ya kufuata nchi ya mlima mrefu na pango la ahadi. Walipofika katikati ya mbuga ya Serengeti, sehemu iitwayo Sanagora walimwona mnyama anayefanana na ng'ombe akija mbiyo akitokea mashariki kuelekea magharibi. Alipowafikia karibu akaanguka nchini na akafa. Punde kidogo walimwona mwindaji akija akafika wakasalimiana naye na wakamwomba huyo mwindaji awapasulie huyo mnyama tumboni mwake, ya kwamba kuna hati zao wanataka wazichukue na kuwa nyama yote achukue. Hiyo ilikuwa mojawapo ya maagizo ya baba yao. Mwindaji huyo hakulikataa ombi lao, hivyo  alimpasua huyo mnyama na humo tumboni walikuta vitu vyao vya utawala vifuatavyo:

i) Zimbura-Mawe ya mvua
ii) Ebherongo-alama avaazo mtemi mikononi na zingine za shingoni
iii) Rigashoda-Ushanga ishara ya amani ya mtawala
iv)Vitu vya usiri vinavyowekwa ndani ya ngoma ya utawala
v) Ekebamba-Chuma cha utawala.

Walipomaliza kuchukua vitu hivyo walimwomba awachunie ngozi na awashonee mifuko ya kubebea vitu hivyo. Alitimiza ombi hilo la wasichana, na hao wasichana waligana naye na mwindaji huyo wakaanza safari kuelekea Sizaki wakiwa na mifuko yao yenye hati za utawala ndani. Walipofika kwenye mlima Changuge hapo walikuta makazi ya mzee mmoja Mhemba aliyeitwa Samong'enya na walikaribishwa vizuri hapo na kupata hifadhi kwa ajiri ya pumziko kwa siku chache huku wakiwa katika mipango ya kuendelea na safari yao. Katika hizo siku chache walizopumzika mawe ya mvua  yaliongezeka yakawa mengi yakawashinda kubeba. Hivyo ilibidi dada mkubwa Wahunda abaki hapo ayachunge. Nyakinywa na Wang'ombe wakiwa na mifuko yao waliendelea na safari yao kuelekea Hunyari. Walifika Hunyari sehemu iitwayo Chahingo, walipumzika kwa muda na bahati nzuri Wang'ombe  aliyekuwamjamzito alijifungua vizuri na akmwomba dada yake amsubiri. Lakini Nyakinywa aliamua kuendelea na safari na kuahidi kumrudia  baada ya kufika mwisho wa safari. Hivyo Wang'ombe alibaki Hunyari.

Nyakinywa alivuka Mto Nyambogo nakupanda milima ya Kihumbu na kuufikia Mlima Nyakinywa akapumzika kidogo, kisha akaendelea na safari yake mpaka mapango ya Gaka. Alipoingia katika pango la Gaka alikanyaga jabali humo ndani lilia kama ngoma  na alipolipiga lilitoa sauti ya ngoma halisi. Hivyo akaelewa kabisa amefika mwisho wa safari yakeakatua mzigo wake kwenye makazi yake mapya  aliyotabiriwa na baba yake. Kesho yake Nyakinywa alitoka  nje ya pango lake akaanza kuchunguza mazingira yake kwa mbali aliona Moshi ulikuwa unatoka mlima Sombayo. Alizidi kuufutia, akavuka Mto Kibangi na kuingia Sombayo ndani ya pango. Punde akatokea mtu mmoja aitwaye mwenye pango hilo  ambaye alikuwa wa ukoo wa Muriho. Samwongo alimuuliza mgeni wake alikuwa anatoka wapi. Nyakinywa alimjibu alikuwa anatoka kwake na kwamba alikuwa amefuata moto. Alimwomba waongozane akaone kwake pia . Waliondoka pamoja mpaka Gaka kwa  Nyakinywa ambapo baada ya kufika na kuwepo na mazungumzo zaidi, Samwongo alimuomba Nyakinywa waoane. Lakini ombi hilo lilikataliwa badala yake waliishi kama wapenzi.

Watu hao wawili waliishi kila mmoja na utaalamu wake. Samwongo alifahamu siri ya kutengeneza na Nyakinywa alikuwa na maji, yaani alikuwa na utaalamu wa kuleta mvua. Kila mmoja alimwomba mwenzake amwonyeshe utaalamu wake lakini hawakukubaliana. Mambo yaliendelea  kuwa hivyo mpaka siku moja Samwongo alikwenda kuwinda, Nyakinywa akaleta mvua kubwa ikamnyeshea mwenzake huko porini akalowa, huku nyumbani mwenzake alizima moto. Aliporudi amelowa sana alikuta moto umezimika pangoni Gaka. Kwa hiyo Samwongo alilazimika amuonyeshe mwenzake namna ya kupata moto. Alitoa kibao cha moto na kijiti chake akapekecha mpaka moto ukatokea hivyo ikawa tayari amemuonyesha Nyakinywa siri ya utengenezaji wa moto. Alimwomba mwenzake naye amuonyeshe siri ya mvua. Nyakinywa hakukataa ombi hilo ila alimwomba mwenzake kwanza amletee dada yake Wang'ombe toka Hunyari, kisha aende porini aue mnyama aitwaye pongo, amchune huko huko aje nyumbani na ngozi peke yake. Samwongo alitimiza yote hayo  kama alivyoagizwa, kesho yake Samwongo aliagizwa atengeneze miti ya kuwambia ngozi hiyo na Samwongo akaitengeneza. Hivyo wakaondoka watu watatu, ngozi ya pongo na miti ya mubamba ngoma kuelekea dimbwi la Nyambogo. Walipofika pale Samwongo aliomba awambe ngozi hiyo juuya maji alijaribu akashindwa. Nyakinywa alijaribu naye ikakubali kukaa juu ya maji. Samwongo aliomba ajaribu mara ya pili na ilikataa pia. Wang'ombe aliombwa ajaribu, yeye alifanikiwa kuwamba ngozi hiyo kama dada yake Nyakinywa. Hivyo Samwongo akaambiwa ameshindwa mtihani hivyo hataoneshwa utaalamu wa kuleta mvua na wakarudi nyumbani Gaka. Wakipofika nyumbani mambo yakageuka yaani Samwongo aliambiwa aoe binti yao ambaye ni binti yake pia. Ingawa mwanzoni alikataa lakini baadae hakuwa na jinsi alikubali  na alimuoa na akawa mkwirima wao na akalazimika kujenga nyumba ya ngoma za utawala hapo nyumbani kwao Gaka. Mwishoni wakamwambia waweke mipaka  kati ya Muriho na Kitang'anyi. Samwongo hakukubaliana na hilo jambo kwa sababu alikuwa na wakubwa zake na ndugu wengine ambao kama ingetokea ilitakiwa ni lazima  washiriki katika jambo kubwa namna hiyo la kugawana utawala wa nchi.

MKUTANO MKUU WA NYAKINYWA NA ABHAKOMBOGERE WA KUMKABIDHI UTAWALA WA NCHI

Baada ya Nyakinywa kutokubaliana kabisa na Samwongo jinsi ya kuigawa nchi na utawala wake ikabidi mkutano mkuu uitishwe toka sehemu kuu mbili zinazohusika kutoa uamuzi wake. Mkutano huo mkuu ulijumuisha makundi makuu mawili kama ifuatavyo:-


  • Abhakombogere
a) Umuchero
b) Nyamau
c) Sibera
d) Chibhora

  • Abharaze
a) Nyakinywa
b) Wahunda
c) Wang'ombe

Kwa ujumla baada ya majadiliano ilikubaliwa kumkaribisha Nyakinywa katika utawala kwa masharti fulani.

MASHARTI

i) Sharti la kwanza ilikuwa la kuleta mvua kuonyesha kweli anao uwezo huo. Nyakinywa alitimiza kwa kufanya mvua inyeshe sana nchi nzima.

ii) Nyakinywa na watu wake walitakiwa kushiriki "uchero". Nyakinywa aliomba kwa kuwa yeye alikuwa Mhima hivyo waungane pamoja na kufanya nyangi ya pamoja na ombi lake lilikubaliwa. Hivyo nyangi hiyo ya ilijumuisha pia makora manane ambayo ni sawa na nyumba nane au hamati nane. Hapo aliomba wagawane nyumba hizi sawa kwa sawa. Abhakombogere walikubaliana na ombi hilo ila wakaweka sharti ya kuwa waruhusiwe kuweka orokobha yaani dawa ya kuzindika nchi nzima hivyo Waraze walikubaliana na tamko hilo.
Abhakombogere pia walimpa Nyakinywa sharti la kuleta mvua nchi nzima ili azime moto wa zamani na waweze kuwasha mwenge au moto mpya. Nyakinywa alikubaliana na ombi hilo la kunyesha mvua "Omosamo" nchi nzima. Masharti yake yote lazima yafuatwe na baadae tutayaona masharti yake hayo aliyowapa. Kwa pamoja mwishoni waliazimia nchi nzima kuwa na makundi au mafiga ambayo yatahusika katika uongozi wa nchi.
Hivyo wakambogere na Waraze (Nyakinywa) wakaungana kuwa kitu kimoja Waikizu wa mwanzo. Nchi nzima ikagawanywa sehemu mbili kufuatana na mkataba wa mkutano mkuu uliotajwa na kuelezewa wa kugawana nyumba nane. Nyakinywa akachukua nne na Abhakombogere wakachukua nne.
Sehemu mbili za nchi zikaitwa Muriho na Kitang'anyi. Nyumba zenyewe zikawa kama ifuatavyo;-

1. Muriho-Nyumba za Nyakinywa zikawa Abharaze (Nyumba za)
a) Abharaze
b) Abhahemba
c) Abhagitiga
d) Abhazera

2. Kitang'anyi- Abhazahya (Nyumba za)
a) Abhazahya
b) Abhamangi
c) Abhasegwe (Abhamanzi/Abhamagenibe)
d) Abhamwanza


IV. MAINGILIO YA WATU WENGINE ZAIDI
Baada ya nyumba nane kugawiwa sehemu mbili
 watu wengi zaidi walizid kuingia toka sehemu mbalimbali na kujiunga aidha kwenye  nyumba ya Abharaze au  abhazahya. Yafuatayo ni maelekezo kwa kifupi kuhusu watu hao:
 
A. UPANDE WA ABHAZAHYA
1. Wamangi-Hao walitokea Busega-Usukumani wakaingia Misarwa Sarama na wakatambulika kwa jina la "Abhamangi".
2. Sinde na Nyawaminza- Hao walitoka Busegwe- Zanaki na kuingia Ketare. Sinde akawa Mzahya na Nyawaminza akajiunga na Wamangi.
3. Wamwanza-Hao wa kwanza walitoka Ikoma na kuingia Sarama, Kongoro na wengine walitokea Zanaki na kujiunga na wenzao wa kutokea Ikoma wote wakawa Wamwanza.
4. Waturi-Hawa walitokea Buzilayombo mpakani mwa Geita na Biharamulo na kuingia Ikizu-Sarama na walipofika wakajiunga na Megabe na Masase wakawa Wazahya.
5. Masase na Megabe- Masase alikuwa Mzahya na Megabe alikuwa mhunzi rafiki yake toka Ntuzu aliyehamia Bumangi wakawa Wahunzi wote na mwishowe wakarudi tena Ikizu na kujiunga na  Wazahya.

B. UPANDE WA WARAZE (ABHARAZE)
1. Waraze-Hao walitoka Kanadi, yaani Nyakinywa na kundi lake.
2. Wahemba-Hao walitokea  Nyarero Waasi (Abhaasi) au Ndorobo na sifa yao kubwa walikuwa ni wawindaji hodari sana. Jamii hii iilikuwa ni kundi kubwa lililosafiri umbali mrefu kwa pamoja na walipofika Mugeta wakagawanyika.
Kundi moja likavuka Mto Tirina na kwenda Nata na wengine wakaingia Mlima Kabohemba uliooko Sarama A. Wengine wakaendelea mpaka Hunyari.
Wengine walitoka Kenya wakiwa na viazi na mitumbwi wakiongozwa na Nyambobhe wakafikia Mozemanga na baada ya ugomvi mzito baina yao na Wamwanza walihamia Mumwaro na Muriho.
Kundi la tatu lilitokea Usukumani wakiwa na mbegu ya mtama na moto wakapitia Changuge, Ushashi na baadae wakajiunga na wenzao wa Ikizu.
3. Wagitiga (Abhagitiga)- Hao wakiongozwa na Chamtigiti walitokea Sonzo sehemu za Arusha na kupitia Ikoma hadi Ikizu. Walikuwa wafugaji wa kondoo na walikuja nambegu za kunde.
4. Wazera (Abhazera)- Hao pia walitokea sehemu za Sonzo Arusha na kupitia Ikoma hadi Ikizu. Jamii hii walikuwa mashuhuri sana katika shughuri ya ufugaji wa nyuki kwa mantiki hiyo miongoni mwa mizigo yao mikubwa waliyokuja nayo ilikuwa ni asali.

*******************************Itaendelea*****************************************

REJEA
Mturi, P. M (2001). Historia ya Ikizu na Sizaki. Goshen College Printing Service. Goshen-Indiana, 
                                                                                                                                                                                                       USA.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni